TANZANIA NI SALAMA, HAKUNA UGONJWA WA MPOX

0

DODOMA

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu ametoa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa wa MPOX na kuwaondoa hofu watanzania kuhusu uwepo wa ugonjwa huo hapa nchini na kuwasisitiza watanzania Kuendelee kuchukua tahadhari.

Prof. Nagu ameyasema hayo leo Agosti 17, 2024 kwenye taarifa aliyoitoa kwa wananchi na kuelezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Afya kufatilia na kuhakikisha ugonjwa huu hauingi nchini na kupata taarifa zote zinazohusu mwenendo wa ugonjwa wa MPOX hapa nchi.

“Mpaka sasa, hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitika kuwa na maambukizi ya Mpox na nchi yetu ni salama, hata hivyo niwasisitize wananchi kuchukua tahadhari kwani tayari shirika la Afya Duniani limetangaza kuwa hili ni janga la dharura.” Amesema Prof. Nagu

Prof. Nagu amesema kuwa kwa sasa nguvu kubwa inaelekezwa kwenye elimu ya kutambua dalili mbalimbali za ugonjwa wa MPOX na itatolewa kwa njia mbalimbali ili iweze kuwafikia wananchi kwa haraka.

“Wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuzuia kuingia nchini ugonjwa wa MPOX na kuimarisha utayari wa kukabiliana nao, hii ni pamoja na kuandaa na kusambaza vipeperushi vya elimu ya jamii kuhusu dalili na njia za kujikinga na ugonjwa wa MPOX, vilevile, wizara imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa ugonjwa huu katika ngazi zote.” Amesema Dkt. Nagu

Aidha Prof. Nagu ameelezea tahadhari mbalimbali za kuchukua ili kujikinga na ugonjwa wa MPOX.

“Tunahitaji kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na ugonjwa huu kwa kutekeleza yafuatayo endapo unamuona mtu anadalili za Mpox, Toa taarifa kwa kupiga simu namba 199 bila malipo, epuka kugusa majimaji ya mwili au ngozi ya mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox, epuka kugusana, kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana na kumbusu mtu mwenye dalili za Mpox, nawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono mara kwa mara, epuka kula au kugusa mizoga au wanyama mfano nyani au swala wa msituni, Vaa barakoa iwapo itabidi kukaa na kuongea kwa karibu na mtu mwenye dalili za Mpox, Kuwahi katika vituo vya huduma za afya unapoona dalili za ugonjwa wa Mpox.” Amesema Prof. Nagu

0 0 votes
Article Rating
Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x