Jeshi la Israel laanzisha operesheni kubwa ya Ukingo wa Magharibi
Inaaminika kuwa ni mara ya kwanza tangu intifada ya pili – uasi mkubwa wa Wapalestina kutoka 2000 hadi 2005 – kwamba miji kadhaa ya Palestina imekuwa ikilengwa kwa wakati mmoja kwa njia hii.
Ripoti za Wapalestina zinasema kuwa, barabara kuu za kuelekea Jenin zimefungwa kutokana na mapigano ya silaha katika kambi ya wakimbizi ya mji huo.
Shambulio la anga la Israel linasemekana kulenga gari katika kijiji jirani alfajiri.
Wanajeshi wa Israel wanasemekana kuingia katika hospitali moja huko Jenin na kuwazuia wawili kutoka Tulkarm.
Uvamizi wa kijeshi wa Israel huko Nablus unaripotiwa kulenga kambi mbili za wakimbizi huko.
Katika kambi ya Far’a karibu na Tubas, madaktari wanasema magari ya kubebea wagonjwa yanatatizika kuwafikia waliojeruhiwa baada ya shambulio la ndege zisizo na rubani za Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje Israel Katz alisema kuwa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) “limekuwa likifanya kazi kwa nguvu zote tangu jana usiku katika kambi za wakimbizi za Jenin na Tulkarm ili kubomoa miundo mbinu ya kigaidi ya Iran na Kiislamu iliyoanzishwa huko”.
Aliishutumu Iran, ambayo inaunga mkono makundi yenye silaha ya Hamas na Palestinian Islamic Jihad, kwa kutaka kufungua kile alichokiita mstari mpya dhidi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
“Lazima tukabiliane na tishio kama vile tunavyoshughulika na miundombinu ya kigaidi huko Gaza, ikiwa ni pamoja na kuwahamisha wakaazi wa Palestina kwa muda na hatua zozote zinazohitajika,” aliongeza.
Jeshi la Israel limetoa maelezo machache lakini lilisema katika taarifa kwamba IDF, wakala wa usalama wa ndani Shin Bet na vikosi vya polisi vya mpakani vya Israel “kwa sasa vinaendesha operesheni ya kukabiliana na ugaidi ili kuzuia ugaidi huko Jenin na Tulkarm”.