Israel inasema miili sita ya mateka wa Hamas ilipatikana
Israel inasema vikosi vyake vimefanikiwa kupata miili sita ya mateka wanaoshikiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa yake, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema miili hiyo ilipatikana siku ya Jumamosi kwenye handaki la chini ya ardhi katika eneo la Rafah.
IDF iliwataja mateka hao kuwa ni Carmel Gat, Eden Yerushalmi, Hersh Goldberg-Polin, Alexander Lobanov, Almog Sarusi na Mwalimu Sgt Ori Danino.
Rais wa Marekani Joe Biden alisema Bw Goldberg-Polin alikuwa raia wa Marekani. “Nimehuzunishwa na kughadhabishwa,” Bw Biden alisema.
Katika taarifa yake Jumapili asubuhi, IDF ilisema miili hiyo “imerejeshwa katika eneo la Israeli”.
“Wote walichukuliwa mateka tarehe 7 Oktoba [2023] na waliuawa na kundi la kigaidi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa familia zao tayari zimearifiwa.
Wakati huo huo, Rais Biden alisema katika taarifa yake kwamba “Hersh alikuwa miongoni mwa watu wasio na hatia walioshambuliwa kikatili alipokuwa akihudhuria tamasha la muziki la amani nchini Israel tarehe 7 Oktoba”.
“Alipoteza mkono wake akiwasaidia marafiki na wageni wakati wa mauaji ya kikatili ya Hamas. Alikuwa ametimiza umri wa miaka 23 tu. Alipanga kusafiri dunia.
“Nimewafahamu wazazi wake, Jon na Rachel. Wamekuwa wajasiri, wenye hekima, na waimara, hata kama wamestahimili mambo yasiyowezekana,” Bw Biden alisema.
Jeshi la Israel lilianzisha kampeni huko Gaza kuharibu Hamas kujibu shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Zaidi ya watu 40,530 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Wapatanishi wa Marekani, Misri na Qatar wanajaribu kusuluhisha makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yatawezesha Hamas kuwaachilia mateka 97 ambao bado wanashikiliwa, wakiwemo takriban 27 wanaodhaniwa wamekufa, ili kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina katika jela za Israel.