Mwanariadha wa Olimpiki Rebecca Cheptegei afariki baada ya shambulio la petroli

0

Mwanariadha wa Olimpiki Rebecca Cheptegei amefariki siku chache baada ya kumwagiwa petroli na kuchomwa moto na mpenzi wake wa zamani, afisa wa Uganda asema.

Mwanariadha huyo wa Uganda wa mbio za marathon mwenye umri wa miaka 33, ambaye alishindana mjini Paris, alijeruhiwa vibaya baada ya shambulio la Jumapili, daktari anayemtibu alisema.

Mamlaka kaskazini-magharibi mwa Kenya, ambako Cheptegei aliishi na kupata mafunzo, walisema alilengwa baada ya kurejea nyumbani kutoka kanisani.

Ripoti iliyowasilishwa na msimamizi wa eneo hilo ilidai kuwa mwanariadha huyo na mpenzi wake wa zamani walikuwa wakizozana kuhusu kipande cha ardhi. Polisi wanasema uchunguzi unaendelea.

Kuna wasiwasi kuhusu ongezeko la visa vya unyanyasaji dhidi ya wanariadha wa kike nchini Kenya, ambavyo vingi vimesababisha vifo.

“Tuna masikitiko makubwa kutangaza kifo cha mwanariadha wetu, Rebecca Cheptegei mapema asubuhi ya leo ambaye aliangukiwa na mzozo wa nyumbani. Kama shirikisho, tunalaani vitendo hivyo na tunaomba haki itendeke. Roho yake ipumzike kwa Amani,” shirikisho la riadha nchini Uganda. alisema katika chapisho kwenye X.

Familia bado haijathibitisha kifo chake lakini Dkt Owen Menach, mkuu wa Hospitali ya Kufundisha na Rufaa ya Moi huko Eldoret, alikokuwa amelazwa, aliambia vyombo vya habari kuwa mwanariadha huyo alifariki baada ya viungo vyake vyote kufeli.

Mpenzi wa zamani wa Cheptegei pia alilazwa hospitalini – lakini akiwa na majeraha ya moto kidogo.

Akiongea na wanahabari, mwanzoni mwa wiki babake, Joseph Cheptegei, alisema kwamba aliomba “haki kwa binti yangu”, akiongeza kuwa hajawahi kuona kitendo hicho cha kinyama maishani mwake.

Kifo chake kinajiri miaka miwili baada ya mauaji ya wanariadha wenza wa Afrika Mashariki Agnes Tirop na Damaris Mutua, huku washirika wao wakitambuliwa kuwa washukiwa wakuu katika visa vyote viwili na mamlaka.

Mumewe Tirop kwa sasa anakabiliwa na mashtaka ya mauaji, ambayo anakanusha, huku msako wa kumtafuta mpenziwe Mutua ukiendelea.

5 1 vote
Article Rating
Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x