Rapa wa Marekani, Maclemore aghairi onyesho la Dubai kuhusu vita vya Sudan
Rapa wa Marekani, Macklemore amesitisha onyesho lake lijalo la mwezi Oktoba huko Dubai, Falme za Kiarabu, kwa madai ya nchi hiyo kuhusika katika mzozo mbaya nchini Sudan.
Alisema watu kwa muda wa miezi kadhaa wamekuwa wakimwomba kusitisha tamasha hilo kwa mshikamano na watu wa Sudan “na kususia kufanya biashara katika UAE kwa jukumu wanalofanya katika mauaji ya kimbari na mgogoro wa kibinadamu unaoendelea katika eneo hilo”.
Rapa huyo alitoa mfano wa taarifa za UAE kuunga mkono Kikosi cha Wanajeshi wa Sudan (RSF), ambacho kimekuwa kikipambana na jeshi la Sudan.
“Hadi UAE itaacha kumiliki silaha na kufadhili RSF sitaigiza huko,” alisema kwenye chapisho kwenye Instagram.
Si jiji la Dubai wala serikali ya UAE iliyotoa maoni kuhusu kauli ya Macklemore.
Mwezi Juni, UAE ilikanusha shutuma kuwa inachochea mzozo huo kama “habari potofu”, ikisema lengo lake lilikuwa katika kupunguza mzozo wa kibinadamu nchini humo.
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Harith Idriss al-Harith Mohamed, alikuwa amesema kwamba msaada wa kifedha na kijeshi wa UAE kwa RSF ndio “sababu kuu ya vita hivi vya muda mrefu”.
Lakini UAE ilisema haya ni “madai ya kejeli” kutoka kwa mwakilishi wa Sudan, “akiwakilisha vikosi vya jeshi, moja ya pande zinazopigana”.
Tangu mapigano hayo yaanze mwezi Aprili mwaka jana, maelfu ya watu wameuawa na milioni 10 kulazimika kuyahama makazi yao.
Vita hivyo vimeibua viwango vya njaa vilivyowahi kurekodiwa duniani , kulingana na Ainisho ya Awamu ya Usalama wa chakula iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa (IPC).
Pande zote mbili zimelaumiwa kwa ukatili lakini RSF imeshutumiwa kutekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya watu wasiokuwa Waarabu katika maeneo ya mkoa wa magharibi wa Darfur ambayo inadhibiti kwa kiasi kikubwa. Imekanusha shtaka hilo, na kuwalaumu wanamgambo wa eneo hilo.
Mazungumzo kadhaa yaliyolenga kumaliza vita vya miezi 16 hadi sasa yameshindwa, huku pande zinazozozana zikiendelea kupigania udhibiti wa nchi hiyo, na hivyo kuzidisha mzozo wa kibinadamu.
Macklemore alisema katika taarifa yake Jumamosi kwamba alichukua uamuzi huo kwa sababu “hali ya sasa nchini Sudan ni ya dharura, ya kutisha na kwa kiasi kikubwa inaenda bila kutambuliwa duniani kote”.
Pia ilitiwa msukumo na vita vya Israel na Hamas vinavyotokea Gaza, anasema, akibainisha kwamba masaibu ya watu wa Palestina “imeamsha ulimwengu”.
Wimbo wa hivi punde zaidi wa msanii aliyeshinda Grammy, Hind’s Hall, unatoa heshima kwa msichana aliyeuawa huko Gaza.
Huko nyuma ametoa muziki unaozungumzia masuala ya kijamii, ikiwa ni pamoja na uraibu wa dawa za kulevya, ulaji na haki za mashoga.
Anasema yeye hawahukumu nyota wengine wanaotumbuiza katika UAE, ambayo mara nyingi huwa mwenyeji wa wasanii wakubwa wa kimataifa na hafla za michezo.
“Lakini ninauliza swali kwa wenzangu waliopangwa kucheza huko Dubai: Ikiwa tungetumia majukwaa yetu kuhamasisha ukombozi wa pamoja, tunaweza kutimiza nini?” aliongeza.