Kesi za Mpox nchini Kenya zafikia 9 wakati juhudi za kudhibiti ugonjwa huo zikiendelea
Wizara ya Afya ya Kenya jana jumatano imethibitisha kesi moja zaidi ya Mpox, na kufanya idadi ya jumla ya kesi za ugonjwa huo kufikia 9 wakati serikali ikiimarisha mwitikio wa afya ya umma kuhusu ugonjwa huo.
Waziri wa Afya wa Kenya Deborah Barasa amesema katika taarifa yake iliyotolewa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi, kwamba kesi hiyo imethibitishwa Nakuru, kilomita 160 kutoka Nairobi, na kuongeza kuwa, mgonjwa huyo mwenye miaka 37 alitembelea nchi za Rwanda na Uganda.
Waziri Barasa amesema, juhudi za ufuatiliaji zinazofanywa na Wizara yake zinaendelea, na watu 68 waliokuwa na mawasiliano ya karibu na wagonjwa wamepatikana, na 61 kati yao wametengwa kwa ajili ya kufuatiliwa kwa karibu kwa siku 21 kama inavyoelekezwa.
Licha ya Kenya, nchi nyingine za Afrika zenye kesi za Mpox ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Burundi, Cameroon, Liberia, Nigeria, Uganda na Rwanda.