Rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili Mongolia, ikiwa ni ziara yake ya kwanza kwa mwanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) tangu ilipotoa kibali cha kukamatwa kwake mwaka jana.
Alikaribishwa na kiongozi wa Mongolia katika hafla ya kifahari katika mji mkuu wa taifa hilo la Asia Ulaanbaatar siku ya Jumanne.
Kiongozi huyo wa Urusi anasakwa na mahakama kwa madai ya kuwafukuza kinyume cha sheria watoto wa Ukraine.
Msemaji kutoka Ikulu ya Kremlin alisema haina wasiwasi kuwa Bw Putin atakamatwa wakati wa ziara hiyo.
Wanajeshi waliopanda farasi walijipanga kwenye Medani ya Genghis Khan ya mji mkuu huo huku nyimbo za kijeshi zikipigwa na bendi ya moja kwa moja kumkaribisha kiongozi huyo wa Urusi, ambaye alikutana na rais wa Mongolia Ukhnaagiin Khürelsükh.
Kikundi kidogo cha waandamanaji walikusanyika katika uwanja huo siku ya Jumatatu alasiri, wakiwa na bango wakidai “Mwondoe Putin Mhalifu wa Kivita hapa”.
Maandamano mengine yanapangwa kufanyika Jumanne adhuhuri katika Mnara wa Ulaanbaatar kwa Waliokandamizwa Kisiasa, ambayo ni kumbukumbu ya wale walioteseka chini ya utawala wa Kikomunisti ulioungwa mkono na Sovieti kwa miongo kadhaa.
Waandamanaji wengine walizuiwa kumkaribia rais wa Urusi alipowasili na vikosi vya usalama.
Kabla ya ziara yake, Ukraine ilikuwa imeitaka Mongolia kumkamata Bw Putin.
“Tunatoa wito kwa mamlaka ya Mongolia kuzingatia hati ya lazima ya kukamatwa kwa kimataifa na kumhamisha Putin kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko Hague,” Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine ilisema kwenye Telegram.
Mahakama hiyo ilidai mwaka jana kuwa rais wa Urusi alihusika na uhalifu wa kivita, ikilenga kuwafukuza kinyume cha sheria watoto kutoka Ukraine hadi Urusi.
Pia imetoa kibali cha kukamatwa kwa kamishna wa haki za watoto wa Urusi, Maria Lvova-Belova, kwa uhalifu huo huo.
Inadai uhalifu huo ulifanyika nchini Ukraine kuanzia tarehe 24 Februari 2022, wakati Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili.
Hapo awali Moscow ilikanusha madai hayo na kusema kuwa vibali hivyo ni vya “chukizo”.
Wanachama wa ICC wanatarajiwa kuwazuilia washukiwa ikiwa hati ya kukamatwa imetolewa, lakini hakuna utaratibu wa utekelezaji.
Mahakama yenye makao yake mjini The Hague wiki iliyopita ilisema wanachama walikuwa na “wajibu” wa kuchukua hatua. Mongolia haijajibu hadharani Ukraine au wito wa ICC.
Jimbo la zamani la satelaiti la Soviet limedumisha uhusiano wa kirafiki na Urusi tangu kuanguka kwa Muungano wa Soviet mnamo 1991.
Haijalaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na imekataa kupigia kura mzozo huo katika Umoja wa Mataifa.
Nchi hiyo isiyo na bandari, ambayo pia inapakana na China, pia inategemea Urusi kwa gesi na umeme.
Urusi imekuwa katika mazungumzo kwa miaka mingi kuhusu kujenga bomba la kubeba gesi asilia mita za ujazo bilioni 50 kwa mwaka kutoka eneo lake la Yamal hadi China kupitia Mongolia.
Mradi huo unaojulikana kwa jina la Power of Siberia 2 , ni sehemu ya mkakati wa kufidia kushuka kwa mauzo ya gesi barani Ulaya, kufuatia kuenea kwa rasilmali za Urusi kutokana na uvamizi wa Ukraine.