Yoon Suk Yeol amekuwa rais wa kwanza wa Korea Kusini kukamatwa baada ya wapelelezi kuweka vizuizi na kukata nyaya ili kumweka kizuizini.
Yoon, mwenye umri wa miaka 64, anachunguzwa kwa madai ya uasi kwa amri iliyofeli ya sheria ya kijeshi mnamo 3 Disemba ambayo iliiingiza nchi katika machafuko.
Pia ameondolewa madarakani na bunge na kusimamishwa kazi – lakini hataondolewa kwenye wadhifa wake hadi Mahakama ya Kikatiba itakapotoa uamuzi kuhusu kushtakiwa kwake.
Kukamatwa kwa Yoon siku ya Jumatano, hata hivyo, kunamaliza mzozo wa wiki moja kati ya wachunguzi na timu yake ya usalama ya rais.
Ofisi ya Uchunguzi wa Ufisadi (CIO) ilikuwa imejaribu kumkamata hapo awali tarehe 3 Januari lakini walizuiliwa na mabasi na nyaya.
Lakini kabla ya mapambazuko siku ya Jumatano, timu ya wachunguzi ilifika, wakiwa na ngazi za kupanda juu ya mabasi na koleo ili kukata waya wenye miiba.
Maafisa wengine katika timu hiyo, ambao walifikia takriban 1,000, walipanda ukuta na kupanda njia za karibu ili kufikia makao ya rais.
Baada ya saa kadhaa, mamlaka ilitangaza kwamba Yoon amekamatwa.
Katika video ya dakika tatu iliyotolewa kabla tu ya kukamatwa kwake, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 64 alisema atashirikiana na wachunguzi, huku akirudia madai yake ya awali kwamba hati hiyo haikuwa halali kisheria.
Alisema alishuhudia jinsi mamlaka “ilivyovamia” eneo la usalama la nyumba yake na vifaa vya moto.
“Niliamua kufika mbele ya CIO, ingawa ni uchunguzi usio halali, ili kuzuia umwagaji wa damu mbaya,” alisema.
Mawakili wa Yoon wamekashifu kukamatwa kwake kuwa ni “haramu” kwa sababu CIO, kama wakala wa kupambana na ufisadi, haina uwezo wa kuchunguza tuhuma za uasi dhidi ya Yoon. Pia wanadai hati hiyo ilitolewa na mamlaka isiyo sahihi.
Hata hivyo, maafisa kutoka mahakama ya juu na wizara ya haki wameshikilia kuwa agizo la kukamatwa lilikuwa halali.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Democratic Party, Park Chan-dae, alisema kukamatwa kwa Jumatano kulionyesha kuwa “haki nchini Korea Kusini iko hai”.
Kukamatwa huku “ni hatua ya kwanza kuelekea kurejesha utaratibu wa kikatiba, demokrasia na utawala wa sheria,” alisema wakati wa mkutano wa chama.
Nchi hiyo kwa sasa inaongozwa na Waziri wa Fedha Choi Sang-mok kama kaimu rais. Aliingizwa madarakani baada ya kaimu rais wa kwanza, Han Duck-soo, pia kushtakiwa na bunge la wengi la upinzani.
Siku ya Jumatano alasiri, wachunguzi walisema kwamba Yoon alikuwa akihojiwa lakini alikuwa ameomba haki ya kunyamaza.
Yoon anatarajiwa kuzuiliwa usiku kucha katika Kituo cha Kizuizi cha Seoul huko Uiwang, Mkoa wa Gyeonggi, takriban kilomita 5 kutoka kwa ofisi ya CIO.
Iwapo mahakama haitatoa kibali cha kuzuiliwa ndani ya saa 48 baada ya Yoon kukamatwa, hata hivyo, ataachiliwa, na kuwa huru kurejea katika makao ya rais.
Wafuasi wa pro-Yoon wameendelea kuandamana kupinga kukamatwa nje ya ofisi ya uchunguzi anakozuiliwa.
Walikuwa wamekusanyika nje ya nyumba ya Yoon Jumatano asubuhi, pamoja na wale wanaompinga.
Umati wa kumpinga Yoon ulishangilia, ukapiga makofi na kulipua wimbo wa “pongezi na sherehe” wakati kukamatwa kwake kulipotangazwa.
Kambi ya pro-Yoon, hata hivyo, ilifadhaika. “Tumesikitishwa sana na tumekasirika – sheria imevunjwa,” mfuasi mmoja aliambia BBC.
Ingawa idadi kubwa ya Wakorea Kusini wanakubali kwamba Yoon lazima awajibike kwa amri ya kijeshi, hawawezi kukubaliana juu ya jinsi uwajibikaji unavyoonekana, Duyeon Kim, msaidizi mwandamizi katika Kituo cha Usalama Mpya wa Amerika aliambia BBC mapema.
Siku ya Jumatano asubuhi, pande hizo mbili zilisisitiza mgawanyiko mkubwa nchini – ishara kwamba mzozo wa kisiasa bado haujaisha kwani kutokuwa na uhakika kunazidi.